Swahili New Testament Bible

Luke 1

Luke

Return to Index

Chapter 2

1


 

  Siku zile, tangazo rasmi lilitolewa na Kaisari Augusto kuwataka watu wote chini ya utawala wake wajiandikishe.  

 

 

-

2


 

  Kuandikishwa huku kulikuwa mara ya kwanza, wakati Kirenio alipokuwa mkuu wa mkoa wa Siria.  

 

 

-

3


 

  Basi, wote waliohusika walikwenda kujiandikisha, kila mtu katika mji wake.  

 

 

-

4


 

  Yosefu pia alifanya safari kutoka mjini Nazareti mkoani Galilaya. Kwa kuwa alikuwa wa jamaa na ukoo wa Daudi alikwenda mjini Bethlehemu mkoani Yuda alikozaliwa Mfalme Daudi.  

 

 

-

5


 

  Alikwenda kujiandikisha pamoja na mchumba wake Maria ambaye alikuwa mja mzito.  

 

 

-

6


 

  Walipokuwa huko, siku yake ya kujifungua ikawadia,  

 

 

-

7


 

  akajifungua mtoto wake wa kwanza wa kiume, akamvika nguo za kitoto, akamlaza horini kwa sababu hawakupata nafasi katika nyumba ya wageni.  

 

 

-

8


 

  Katika sehemu hizo, walikuwako wachungaji wakikesha usiku mbugani kulinda mifugo yao.  

 

 

-

9


 

  Malaika wa Bwana akawatokea ghafla, na utukufu wa Bwana ukawaangazia pande zote. Wakaogopa sana.  

 

 

-

10


 

  Malaika akawaambia, "Msiogope! Nimewaleteeni habari njema ya furaha kuu kwa watu wote.  

 

 

-

11


 

  Kwa maana, leo hii katika mji wa Daudi, amezaliwa Mwokozi kwa ajili yenu, ndiye Kristo Bwana.  

 

 

-

12


 

  Na hiki kitakuwa kitambulisho kwenu: mtamkuta mtoto mchanga amevikwa nguo za kitoto, amelazwa horini."  

 

 

-

13


 

  Mara kundi kubwa la jeshi la mbinguni likajiunga na huyo malaika, wakamsifu Mungu wakisema:  

 

 

-

14


 

  "Utukufu kwa Mungu juu mbinguni, na amani duniani kwa watu aliopendezwa nao!"  

 

 

-

15


 

  Baada ya hao malaika kuondoka na kurudi mbinguni, wachungaji wakaambiana: "Twendeni moja kwa moja mpaka Bethlehemu tukalione tukio hili Bwana alilotujulisha."  

 

 

-

16


 

  Basi, wakaenda mbio, wakamkuta Maria na Yosefu na yule mtoto mchanga amelazwa horini.  

 

 

-

17


 

  Hao wachungaji walipomwona mtoto huyo wakawajulisha wote habari waliyokuwa wamesikia juu yake.  

 

 

-

18


 

  Wote waliosikia hayo walishangaa juu ya habari walizoambiwa na wachungaji.  

 

 

-

19


 

  Lakini Maria aliyaweka na kuyatafakari mambo hayo yote moyoni mwake.  

 

 

-

20


 

  Wale wachungaji walirudi makwao huku wakimtukuza na kumsifu Mungu kwa yote waliyokuwa wamesikia na kuona; yote yalikuwa kama walivyokuwa wameambiwa.  

 

 

-

21


 

  Siku nane baadaye, wakati wa kumtahiri mtoto ulipofika, walimpa jina Yesu, jina ambalo alikuwa amepewa na malaika kabla hajachukuliwa mimba.  

 

 

-

22


 

  Siku zilipotimia za Yosefu na Maria kutakaswa kama walivyotakiwa na Sheria ya Mose, wazazi hao walimchukua mtoto, wakaenda naye Yerusalemu ili wamweke mbele ya Bwana.  

 

 

-

23


 

  Katika Sheria ya Bwana imeandikwa: "Kila mzaliwa wa kwanza wa kiume atawekwa wakfu kwa Bwana."  

 

 

-

24


 

  Pia walikwenda ili watoe sadaka: hua wawili au makinda wawili ya njiwa, kama ilivyotakiwa katika Sheria ya Bwana.  

 

 

-

25


 

  Wakati huo huko Yerusalemu kulikuwa na mtu mmoja, mwema na mcha Mungu, jina lake Simeoni. Yeye alikuwa akitazamia kwa hamu ukombozi wa Israeli. Roho Mtakatifu alikuwa pamoja naye.  

 

 

-

26


 

  Roho Mtakatifu alikuwa amemhakikishia kwamba hatakufa kabla ya kumwona Masiha wa Bwana.  

 

 

-

27


 

  Basi, akiongozwa na Roho Mtakatifu, Simeoni aliingia Hekaluni; na wazazi wa Yesu walipomleta Hekaluni mtoto wao ili wamfanyie kama ilivyotakiwa na Sheria,  

 

 

-

28


 

  Simeoni alimpokea mtoto Yesu mikononi mwake huku akimtukuza Mungu na kusema:  

 

 

-

29


 

  "Sasa Bwana, umetimiza ahadi yako, waweza kumruhusu mtumishi wako aende kwa amani.  

 

 

-

30


 

  Maana kwa macho yangu nimeuona wokovu utokao kwako,  

 

 

-

31


 

  ambao umeutayarisha mbele ya watu wote:  

 

 

-

32


 

  Mwanga utakaowaangazia watu wa mataifa, na utukufu kwa watu wako Israeli."  

 

 

-

33


 

  Baba na mama yake Yesu walikuwa wakistaajabia maneno aliyosema Simeoni juu ya mtoto.  

 

 

-

34


 

  Simeoni akawabariki, akamwambia Maria mama yake, "Mtoto huyu atakuwa sababu ya kupotea na kuokoka kwa watu wengi katika Israeli. Naye atakuwa ishara itakayopingwa na watu;  

 

 

-

35


 

  na hivyo mawazo ya watu wengi yataonekana wazi. Nawe mwenyewe, uchungu ulio kama upanga mkali utauchoma moyo wako."  

 

 

-

36


 

  Palikuwa na nabii mmoja mwanamke, mzee sana, jina lake Ana, binti Fanueli, wa kabila la Asheri. Alikuwa ameishi na mumewe kwa miaka saba tangu alipoolewa.  

 

 

-

37


 

  Halafu alibaki mjane hadi wakati huo akiwa mzee wa miaka themanini na minne. Wakati huo wote alikaa Hekaluni akifunga na kusali usiku na mchana.  

 

 

-

38


 

  Saa hiyohiyo alijitokeza mbele, akamshukuru Mungu, na akaeleza habari za huyo mtoto kwa watu wote waliokuwa wanatazamia ukombozi wa Yerusalemu.  

 

 

-

39


 

  Hao wazazi walipokwisha fanya yote yaliyoamriwa na Sheria ya Bwana, walirudi makwao Nazareti, mkoani Galilaya.  

 

 

-

40


 

  Mtoto akakua, akazidi kupata nguvu, akajaa hekima, na neema ya Mungu ilikuwa pamoja naye.  

 

 

-

41


 

  Wazazi wa Yesu walikuwa na desturi ya kwenda Yerusalemu kila mwaka wakati wa sikukuu ya Pasaka.  

 

 

-

42


 

  Mtoto alipokuwa na umri wa miaka kumi na miwili, wote walikwenda kwenye sikukuu hiyo kama ilivyokuwa desturi.  

 

 

-

43


 

  Baada ya sikukuu, walianza safari ya kurudi makwao, lakini Yesu alibaki Yerusalemu bila wazazi wake kuwa na habari.  

 

 

-

44


 

  Walidhani alikuwa pamoja na kundi la wasafiri, wakaenda mwendo wa kutwa, halafu wakaanza kumtafuta miongoni mwa jamaa na marafiki.  

 

 

-

45


 

  Kwa kuwa hawakumwona, walirudi Yerusalemu wakimtafuta.  

 

 

-

46


 

  Siku ya tatu walimkuta Hekaluni kati ya walimu, akiwasikiliza na kuwauliza maswali.  

 

 

-

47


 

  Wote waliosikia maneno yake walistaajabia akili yake na majibu yake ya hekima.  

 

 

-

48


 

  Wazazi wake walipomwona walishangaa. Maria, mama yake, akamwuliza, "Mwanangu, kwa nini umetutenda hivyo? Baba yako na mimi tumekuwa tukikutafuta kwa huzuni."  

 

 

-

49


 

  Yeye akawajibu, "Kwa nini mlinitafuta? Hamkujua kwamba inanipasa kuwa katika nyumba ya Baba yangu?"  

 

 

-

50


 

  Lakini wazazi wake hawakuelewa maana ya maneno aliyowaambia.  

 

 

-

51


 

  Basi, akarudi pamoja nao hadi Nazareti, akawa anawatii. Mama yake akaweka mambo hayo yote moyoni mwake.  

 

 

-

52


 

  Naye Yesu akaendelea kukua katika hekima na kimo; akazidi kupendwa na Mungu na watu.  

 

 

-

Luke 3

 

 

 

 

HTMLBible Software - Public Domain Software by johnhurt.com

 


Other Items are Available At These Sites: