Swahili New Testament Bible

Matthew 28

Mark

Return to Index

Chapter 1

1


 

  Habari Njema ya Yesu Kristo, Mwana wa Mungu.*fa*  

 

 

-

2


 

  Ilianza kama ilivyoandikwa katika kitabu cha nabii Isaya: "Tazama, namtuma mjumbe wangu akutangulie; yeye atakutayarishia njia yako.  

 

 

-

3


 

  Sauti ya mtu imesikika jangwani: `Mtayarishieni Bwana njia yake, nyoosheni mapito yake."`  

 

 

-

4


 

  Yohane Mbatizaji alitokea jangwani, akahubiri kwamba ni lazima watu watubu na kubatizwa ili Mungu awasamehe dhambi zao.  

 

 

-

5


 

  Watu kutoka sehemu zote za Yudea na wenyeji wote wa Yerusalemu walimwendea, wakaziungama dhambi zao, naye akawabatiza katika mto Yordani.  

 

 

-

6


 

  Yohane alikuwa amevaa vazi lililofumwa kwa manyoya ya ngamia, na mkanda wa ngozi kiunoni mwake. Chakula chake kilikuwa nzige na asali ya mwituni.  

 

 

-

7


 

  Naye alihubiri akisema, "Baada yangu anakuja mwenye uwezo zaidi kuliko mimi, ambaye mimi sistahili hata kuinama na kufungua kamba za viatu vyake.  

 

 

-

8


 

  Mimi ninawabatiza kwa maji, lakini yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu."  

 

 

-

9


 

  Siku hizo, Yesu alifika kutoka Nazareti, mji wa Galilaya, akabatizwa na Yohane katika mto Yordani.  

 

 

-

10


 

  Mara tu alipotoka majini, aliona mbingu zimefunguliwa, na Roho akishuka juu yake kama njiwa.  

 

 

-

11


 

  Sauti ikasikika kutoka mbinguni: "Wewe ni Mwanangu mpendwa, nimependezwa nawe."  

 

 

-

12


 

  Mara akaongozwa na Roho kwenda jangwani,  

 

 

-

13


 

  akakaa huko siku arubaini akijaribiwa na Shetani. Alikuwa huko pamoja na wanyama wa porini, nao malaika wakawa wanamtumikia.  

 

 

-

14


 

  Yohane alipokwisha fungwa gerezani, Yesu alikwenda Galilaya, akahubiri Habari Njema ya Mungu, akisema,  

 

 

-

15


 

  "Wakati umetimia, na Ufalme wa Mungu umekaribia. Tubuni na kuiamini Habari Njema!"  

 

 

-

16


 

  Alipokuwa anapita kando ya ziwa Galilaya, aliwaona wavuvi wawili: Simoni na Andrea ndugu yake wakivua samaki kwa wavu.  

 

 

-

17


 

  Yesu akawaambia, "Nifuateni nami nitawafanya ninyi wavuvi wa watu."  

 

 

-

18


 

  Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata.  

 

 

-

19


 

  Alipokwenda mbele kidogo, aliwaona Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo. Nao pia walikuwa ndani ya mashua yao wakizitengeneza nyavu zao.  

 

 

-

20


 

  Yesu akawaita mara, nao wakamwacha baba yao Zebedayo katika mashua pamoja na wafanyakazi, wakamfuata.  

 

 

-

21


 

  Wakafika mjini Kafarnaumu, na mara ilipofika Sabato, Yesu akaingia katika Sunagogi, akaanza kufundisha.  

 

 

-

22


 

  Watu wote waliomsikia walishangazwa na mafundisho yake, maana hakuwa anafundisha kama walimu wao wa Sheria, bali kama mtu mwenye mamlaka.  

 

 

-

23


 

  Mara akatokea mle ndani ya sunagogi mtu mmoja mwenye pepo mchafu,  

 

 

-

24


 

  akapaaza sauti, "Una nini nasi, wewe Yesu wa Nazareti? Je, umekuja kutuangamiza? Najua wewe ni nani: wewe ni Mtakatifu wa Mungu!"  

 

 

-

25


 

  Yesu akamkemea, "Nyamaza! Mtoke mtu huyu."  

 

 

-

26


 

  Basi, huyo pepo mchafu akamtikisatikisa mtu huyo, kisha akalia kwa sauti kubwa, akamtoka.  

 

 

-

27


 

  Watu wote wakashangaa, wakaulizana, "Ni mambo gani haya? Je, ni mafundisho mapya? Mtu huyu anayo mamlaka ya kuamuru hata pepo wachafu, nao wanamtii!"  

 

 

-

28


 

  Habari za Yesu zikaenea upesi kila mahali katika wilaya ya Galilaya.  

 

 

-

29


 

  Wakatoka katika sunagogi, wakaenda moja kwa moja hadi nyumbani kwa Simoni na Andrea; Yakobo na Yohane walikwenda pamoja nao.  

 

 

-

30


 

  Basi, mama mmoja, mkwewe Simoni, alikuwa kitandani ana homa kali. Wakamwarifu Yesu mara alipowasili.  

 

 

-

31


 

  Yesu akamwendea huyo mama, akamshika mkono, akamwinua. Na ile homa ikamwacha, akaanza kuwatumikia.  

 

 

-

32


 

  Jioni, jua lilipokwisha tua, wakamletea Yesu wagonjwa wote na watu waliopagawa na pepo.  

 

 

-

33


 

  Watu wote wa mji ule wakakusanyika nje ya mlango.  

 

 

-

34


 

  Naye Yesu akawaponya watu wengi waliokuwa na magonjwa mbalimbali; aliwafukuza pepo wengi, lakini hakuwaruhusu kusema kitu maana walikuwa wanamjua yeye ni nani.  

 

 

-

35


 

  Kesho yake, kabla ya mapambazuko, Yesu alitoka, akaenda mahali pa faragha kusali.  

 

 

-

36


 

  Simoni na wenzake wakaenda kumtafuta.  

 

 

-

37


 

  Walipomwona wakamwambia, "Kila mtu anakutafuta."  

 

 

-

38


 

  Yesu akawaambia, "Twendeni katika miji mingine ya jirani nikahubiri huko pia, maana nimekuja kwa sababu hiyo."  

 

 

-

39


 

  Basi, akaenda kila mahali Galilaya akihubiri katika masunagogi na kufukuza pepo.  

 

 

-

40


 

  Mtu mmoja mwenye ukoma alimwendea Yesu, akapiga magoti, akamwomba, "Ukitaka, waweza kunitakasa!"  

 

 

-

41


 

  Yesu akamwonea huruma, akanyosha mkono wake, akamgusa na kumwambia, "Nataka, takasika!"  

 

 

-

42


 

  Mara ukoma ukamwacha mtu huyo, akatakasika.  

 

 

-

43


 

  Kisha Yesu akamwambia aende zake upesi na kumwonya vikali,  

 

 

-

44


 

  "Usimwambie mtu yeyote jambo hili, ila nenda ukajionyeshe kwa kuhani; kisha utoe sadaka kwa ajili ya kutakasika kwako kama alivyoamuru Mose, iwe uthibitisho kwao kwamba umepona."  

 

 

-

45


 

  Lakini huyo mtu akaenda, akaanza kueneza habari hiyo kila mahali na kusema mambo mengi hata Yesu hakuweza tena kuingia katika mji wowote waziwazi; ikamlazimu kukaa nje, mahali pa faragha. Hata hivyo, watu wakamwendea kutoka kila upande.  

 

 

-

Mark 2

 

 

 

 

HTMLBible Software - Public Domain Software by johnhurt.com

 


Other Items are Available At These Sites: